Alhamisi, 15 Februari 2024

SEMINA YA NENO LA MUNGU UWANJA WA RELI-ARUSHA: NA MWL. CHRISTOPHER  MWAKASEGE

SIKU YA PILI : 11 JANUARI, 2024 SOMO : MALENGO MKAKATI YA KUFANIKISHA MIPANGO YAKO LINK YA SOMO LA HILI YOUTUBE 👇🏼                                         https://www.youtube.com/live/aEiFAFxT__g8?si=odxQ9pqravFfCeGf  NAMBA ZA KUTUMA SADAKA, MAOMBI NA SHUHUDA 👇🏼  https://bit.ly/Sadaka-Maombi-Shuhuda  KUJIUNGA GROUP LA TELEGRAM: 👇🏼  https://t.me/Mwakasegemanaministry   UTANGULIZI  MALENGO YA SOMO Katika somo hili tuna malengo makubwa mawili. 1. Kukumbusha juu ya umuhimu wa malengo mkakati ya Kibiblia yaliyowekwa ili kubeba mipango kimafanikio. 2. Kukujulisha namna ya kugeuza lengo la kawaida kuwa lengo mkakati linalotekelezeka na linalofikika. Yerema 29:11 “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.” Katika tafsiri nyingine wamesema siku zenu za baadae lakini katika kiingereza wamesema Jeremiah 29:11 NIV “For I know the plans I have for you,” declares the Lord, “plans to prosper you and not to harm you, plans to give you hope and a future.” Ayubu 22:21 “Mjue sana Mungu, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia.” Kama mpango wako ni kumjua Mungu kwa mwaka huu unatakiwa kuweka mikakati ya kumjua Mungu mana ndio inakuja kubeba vingine vyote.  Ngoja tuone tofauti ya lengo mkakati na mpango mkakati: Watu wengi wana mipango na wana mikakati ya vitu vya kufanya bila malengo. Na kwa sababu hiyo ukiwauliza mwaka huu katika jambo wanalofanya wamekusudia kufika mpaka wapi, hawana jibu. Au mwingine atakuambia ni kwa kadri Mungu atakavyomwezesha.  Inaweza ikawa ni jibu lakini si jibu sahihi sana kwa sababu utaona hajui mahali ambapo Mungu amekusudia amfikishe.  MFANO: Ukiwa kwenye mpango wako wa kufanikiwa na ukafungua duka na ukaamua kuuza vitu hapo, lengo lako ni nini? Je! Ni kuuza vitu tu au kupata hela?  Kwa sababu kuna watu wanafurahia kwamba vitu vimeisha dukani bila kujua wamepata shilingi ngapi. Kwani ikifika mwisho wa mwaka atasema hajui kwa nini mtaji wake umekata. Hiyo ni kwa sababu hakuweka malengo ya kupata kitu kutoka kwenye duka hilo na umeenda hivyo miaka mingi bila kuwa na mafanikio kipesa.  Sasa kama Mungu amekupa lengo ndani yake ataweka na mkakati wa kukusaidia ili uweze kufikia lengo hilo. Na utakuja kujua kama umemjua Mungu kwa kiasi gani (kidogo, wastani au kikubwa). Itakuwa vigumu sana kujipima mwenyewe lakini ukishaanza kujifunza juu ya mikakati itakusaidia kwa namna ambayo itakuongezea kiu.  MIKAKATI YA KUMJUA MUNGU ILI IKUSAIDIE KUWEKA KATIKA MALENGO YAKO YA MWAKA HUU NA KATIKA MAISHA YAKO MKAKATI WA KWANZA FAHAMU KUNATOKEA NINI KWAKO UNAPOMJUA MUNGU Ufahamu utakuongezea kiu ya kumjua Mungu kwa kina zaidi bila kitu chochote kuingia katikati hapo kukukwamisha kutekeleza mkakati huo.  Wafilipi 3:7-10 “Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo; tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa imani; ili nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso yake, nikifananishwa na kufa kwake;” Tujiulize kwa nini amesema mambo yote amehesabu kuwa hasara?  Haina maana kwamba kila kitu alichofanya kilikuwa kibaya, bali amejisemesha mwenyewe kuwa hasara ya kitu anachokifanya haiwezi kubadilisha nafasi aliyompa Mungu maishani mwake. Hata kama anapata faida lakini Yesu akapoteza nafasi anayostahili, vitu vingine vyote ni hasara.  Kuna kitu amekiona kuhusu uzuri usio na kiasi wa kumjua Yesu Kristo Bwana wake.  Kuna uzuri fulani yeye ameuona na sisi wengine hatuuoni ingawa anajaribu kutueleza mpaka anaongea maneno mazito hayo.  Kwa tafsiri nyingine anamaanisha: “KUMJUA YESU KRISTO BWANA WAKE NI BORA ZAIDI KULIKO KUMTUMIKIA”  Kama kumtumikia Mungu kumechukua nafasi ya kwanza kuliko kumjua Yeye aliyekupa hiyo kazi, ujue kuna shida mahali. Kama faida na kufanikiwa kwako kutanyang`anya nafasi ya ushirika na Mungu.  Swali ambalo utakuwa unajiuliza kuwa ni kitu gani kinatokea unapomjua Mungu. Paulo alipata kitu kikubwa kuliko vitu vingine vyote. Leo tunatazama vitu ambavyo vinatokea ukimjua Mungu. KITU CHA KWANZA KUMJUA MUNGU KUNAKUBADILISHA WEWE NI NANI NDANI YAKO NA NJE YAKO Danieli 11:32b Lakini watu wamjuao Mungu wao watakuwa hodari, na kutenda mambo makuu. Hapa nataka uangalie sana lile neno, watu wamjuao Mungu watakuwa. Kabla hawajamjua Mungu hawakuwa. Knowing God changes you. Ukimjua Mungu inakubadilisha wewe ni nani, kunakubadilisha ndani. Watu wanakuwa hawana namna ya kukuuliza kuwa ni kitu gani kimetokea. Lakini watajua kwa nje maana utatenda mambo makuu. Hawatajua namna unavyotenda bali watajua unachotenda. Japo kuna wengine watataka kucopy namna unavyofanya lakini hawataweza kucopy unavyofanya. Maana unavyotenda inatokana na yule aliye ndani yako. Paulo alikuja kugundua kuwa anachofanya kinatokana na yule ambaye anamjua ambaye anataka awe kama anavyotaka, na ya kuwa anachofanya kitakuwa ni hasara tupu kama hamjui huyo ambaye anatakiwa kumbadilisha ndani ili awe anavyotaka awe ili sasa aweze kufanya kwa namna ambavyo anataka afanye ili apate matokeo ambayo anayataka.  Kwa hiyo kama hajambadilisha, hicho kitu anachokifanya ni hasara. Hii itakusaidia sana kila mara unapoingia katika maandiko na kusoma mstari wa kumjua Mungu. Fuatilia kitu gani kinatokea unapomjua Mungu. Kama hakijatokea kwako basi ujue bado hujamjua Mungu. Kuna picha Mungu alikuwa nayo alipotuleta Duniani, alitupa sura yake, mfumo wake, mamlaka yake na kitu cha kufanya. Dhambi ilipoingia ilitubadilisha tuliyokuwa na tukabadilika  tunavyofanya. Kwa hiyo ni lazima uokoke uwe kiumbe kipya, maana huwezi kusimama katika ile nafasi ambayo Mungu amekupa, maana kuna nafasi nyingine unapewa na msalaba na neema.  Huwezi ukamjua Mungu bila kumjua Kristo. Yesu alisema aliyeniona mimi amemuona baba.  Kazi inaweza kuwa ile ile unayoifanga lakini kadri unavyomjua Mungu mwaka huu kiwango chako kikiongezeka utendaji wako utabadilika kabisa. Hiki ni kitu kinatoka ndani, maana kiu ya kuona ufanisi unaongezeka inakuwa ni kiu yako ya ndani. Mtu wa ndani ndio anakuwa na vigezo vyake vya ufanisi, maana ndani yake ndiko Mungu kaweka viwango na vigezo vya ufanisi. Na huyo ndio ataamua kuwa hatuwezi kuendelea kwa staili hii. Je umewahi kuona nguo mpya zipo katika mitumba, maana yake kama umeona hizo nguo basi tambua ya kuwa zimekosa kiwango na ndio maana zipo hapo katika mitumba. Wewe unaweza usijue lakini kama hicho kitu kimekosa kiwango kinakuwa reject na kwenda katika mtumba au tabaka la chini kidogo. Huyu mtu ambaye Mungu anamtengeneza ndani yako kuna viwango Mungu anaweka. Sasa kuna watu ambao watapenda mtumba lakini wapo ambao watadaka na kufurahia viwango vipya. KITU CHA PILI KUMJUA MUNGU KUNABADILISHA VITU UNAVYOKUWA NAVYO NDANI YAKO NA NJE YAKO Ayubu 22:21** “Mjue sana Mungu, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia.” Kumjua Mungu kunaweka vitu ndani yako na kukubadilisha wewe. Biblia inasema kadri unavyozidi kumjua Mungu ndivyo amani inaongezeka. Isaya 9:6 “Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani.” Si tu kwamba Yesu anakubadilisha na kuwa mtu mwingine ila pia ataweka kitu cha kusaidiana naye ambayo mojawapo ni amani.  Kazi kubwa ya amani ni kutawala roho yako na maamuzi yako. Sasa watu wengi sana wakitaka kufanikiwa hawafuati mifumo ya kimafanikio. Mafanikio yako yanategemea nani yupo kwenye mifumo ndio maana watu wengi sana waliookoka wakiingia kwenye mifumo kiroho chao kinapoa kwa kutokumjua Mungu sana ili wawe na amani ambayo italinda maamuzi yao.  Wafilipi 4:6-7 “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.” Baada ya kuingia kwa dhambi duniani ukishaanza kufanikiwa shetani asingependa kuona watu wa Mungu wanaanza kufanikiwa na ndio malengo yake popote iwe kazini au ndani ya familia yako. Shetani anataka Mungu asipate heshima yake kwa kuonyesha kuwa ameshindwa kuwatetea watu wake.  Ukiomba Mungu akufanikishe atakupa maelekezo hiyo ni baada ya kuwa na amani inakupa utulivu na usikivu ndani yako.  sawa na  Isaya 1:19 “Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi;” Kwa hiyo lazima tuwe na kifungo cha amani na Mungu atatupa watu wa kushirikiana nao kila sehemu na katika miji mbalimbali na hata tunapoishi. Usichague wa kuambatana nao kwa kuwatazama. Unaweza kukwama kabisa.  Saa nyingine wengi wanachaguana kwa sababu ya kuokoka kwao.  Mfano mnachaguana kufanya biashara pamoja kwa sababu mmeokoka. Hicho kigezo hakitoshi.  Unaweza ukakuta ameokoka na hakuitiwa kufanya biashara kumbe ni mkulima kabisa sasa unajikuta wewe unabeba kila kitu.  Muda mwingine mkikaa kwenye kikao cha bodi mwanzo hadi mwisho hukuti akiwa na mchango zaidi ya kusema “NDIYO”. Akiulizwa labda ana neno lolote atasema “HAPANA, LAKINI FULANI UNAJUA AMETOA WAZO ZURI SANA MIMI NAFIKIRI TUKUBALIANE NAYE”. Mwisho wa mwaka anapokea gawio lake halafu unaanza kukosa amani bila kujua kakukosea nini. Muda mwingine watu wanakuwa waoga kufanya maamuzi sahihi na mambo yao mengi kukwama. Hiyo ni kwa sababu umembeba Yona wako kwenye boti lako. Utapata hasara tu kutokana na mengi kuharibika au umeyaacha njiani.  Muhimu sasa umjue Mungu sana ili vitu vya namna hii visitokee ili usikose mema yako.  Neno linaposema “NDIVYO MEMA YATAKAVYOKUJIA” humaanisha mtiririko wa mema kuja kwako kwa mfululizo. Yaani Mungu anakufungulia yote na si muujiza mmoja mmoja kwa muda mrefu.  MFANO: Fikiria kwa mwezi unapata TShs laki sita halafu sasa Mungu anakuambia kuanzia sasa kila siku nakupa TShs laki sita (TShs 600,000) sawasawa na Kumb. 28 : 1 - 14. Sasa nakuuliza Je! Moyo wako una uwezo wa kubeba hiyo laki sita?  Kwa sababu hizo baraka zimeamriwa kukufuata na kukupata.  Maana yake zitakufuata (ukijaribu kukwepa, umelala, umeamka, unafurahi, una hasira n.k.. zinakuja). Na watu wanaotumia nguvu za giza watasema wewe utakuwa mchawi sana kumbe wewe umemjua sana Mungu wako.  Muda mwingine ni rahisi sana kusema kikombe changu kinafurika (sawa, inaweza kuwa ni kipimo chako) unakuja kugundua watu wengine wanakuja kufaidi kuliko wewe kutokana na kibebeo chako kuwa ndogo. Sasa Mungu anakuja kukupa namna ya kuchukulia kipimo hicho.  Mungu anapokuja kwako anakuja kukuwekea utulivu na amani ya kupokea maelekezo anayokupa ili upate imani ya kufika kule alikokupangia.  JAMBO LA TATU LINALOTOKEA KWAKO UNAPOMJUA YESU KUMJUA MUNGU KUNAONGEZA UWEZA WA MOYO WAKO WA KUMBEBA YESU ALIVYO MOYONI MWAKO NA KWA AJILI YAKO Marko 4:35 - 41 “Siku ile kulipokuwa jioni, akawaambia, Na tuvuke mpaka ng’ambo. Wakauacha mkutano, wakamchukua vile vile alivyo katika chombo. Na vyombo vingine vilikuwako pamoja naye. Ikatokea dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji. Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia? Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu. Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado? Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?” Hawa watu hawakutakiwa wambebe Yesu kwenye boti tu bali wambebe na mioyoni mwao kwanza ndio wamwingize kwenye boti lao. Utajua hili baada ya wao kumwamsha na Yeye kuwauliza kuwa “HAWANA IMANI BADO?”  Kuna imani walitakiwa kuwa nayo kabla hawajakutana na dhoruba. Aliwaelewesha juu ya imani wanayopaswa kuwa nayo ila wakazoea yale mazingira ya bahari ya kutokuwa na mawimbi iwe mchana au usiku.  Ila sasa katika Marko 2: 1 - 12 utaona habari za mtu aliyepooza na watu kadhaa walimbeba ili aponywe na Yesu. Wakafungua dari na kumteremsha hadi alipo Yesu. Sasa Yesu alipoiona imani ya wale watu (si imani ya mgonjwa) akaachilia neno la uponyaji. Yesu aliona imani yao ikitoka mioyoni mwao na imani hiyo ikambeba mikononi mwao aliyepooza kwa hiyo moyo ndio uliokuwa umembeba aliyepooza. Moyo ulipombeba ukaelekeza mikono yao na hatua zao.  Kwenye Marko Yesu alipowauliza kuwa hawana imani bado ukilinganisha na hii hawa waliombeba aliyepooza unaona vitu viwili tofauti.  Ndipo Yesu akasema aliyepooza amesamehewa dhambi zake kwa sababu imani yao ilionekana mbele za Mungu.  Hata kama hujui kujieleza imani yako na matendo yako vitaonekana mbele za Mungu.  Wale wenye mashaka ndipo Yesu akawaambia kipi kigumu kwake? Kwa sababu anaweza kusamehe dhambi, ya aliyepooza akanyanyuka baada ya kuambiwa amesamehewa dhambi, akasimama na kuondoka.  Ndipo unakuja kuona swali la wanafunzi “Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?” Ukikata katikati hiyo sentensi utaona vitu viwili: 1. Imani yao kwa Yesu (Yesu ni nani kwao) [Ni nani huyu].  2. Imani inayosimama kwenye matendo [hata upepo na bahari humtii?].  Je Yesu alikuwa anatafuta imani gani? Maana ile kwamba wale watu wameacha kila kitu na wameamua kumfuata Yesu ina maana walikuwa na imani naye. Lakini swali la Yesu alikuwa alipouliza je hamna imani bado maana yake kuna imani nyingine ambayo alikuwa anaitafuta.  Hapa ina maananisha kuwa hawa watu walikuwa na imani ambayo katika mazingira yale ilikuwa haina msaada kwao. Ni muhimu sana uwe na imani ambayo inashughulika na mazingira yako uliyonayo.  Hili swali Yesu aliwauliza kuwa je watu huko mtaani wanasema mimi ni nani?  Na je nyie mnasema mimi ni nani? Walimuona Yesu ng’ambo ya pili akikemea pepo lakini wameingia katika boti hawamjui tena huyu Yesu. Kwa hiyo hawakuweza kumuamini. Ukimjua Mungu anakuja ndani ya moyo wako. Ndani ya moyo wako dhambi ilipoingia, ilimuondoa Yesu na ikapunguza vitu vingine. Lakini sasa ukianza kumjua Yesu ile imani ndani yako kuna vitu inaanza kuingiza ya kumjua yeye ni nani. Kwa hiyo hali ya namna hiyo itaanza kudai nafasi. Sasa Yesu alipowauliza swali wanafunzi wake mbona mmekuwa waoga, ina maana kuna mahali imani yao ilitakiwa ikae katika nafasi kama hiyo lakini haikukaa na inaonesha kulikuwa na kitu kingine pale. Je katika mazingira ya mwaka 2024 Yesu ni nani kwako.  Kama kuna mahali unapita na mahali unapopita ni papya, unajikuta unapata hofu. Tunakuuliza kwa nini unakuwa mwoga unasema  Yesu ninaye. Lakini kwa kweli kuna imani ulitakiwa uwe nayo na sasa hauna. Ni kwa sababu hujamjua Yesu kuwa ni nani katika eneo hilo. Yesu anaingia ndani yako na kufanya uwe na imani maalumu yaani ya kumbeba moyoni mwako. Wale wanafunzi walikuwa wamembeba Yesu katika chombo na hawakumbeba moyoni mwao. Maana wangembeba moyoni mwao wasingekuwa na hofu. Amani ambayo Mungu anakupa haijalishi yapo mawimbi kama yapo au hayapo bado unakuwa na amani ndani yako. Ndani yako kukijaa Kristo ambaye unamjua unakuwa hauna hofu. Yesu aliingia katika boti na uwezo wake aliokua nao ulikuwa ni kwa ajili yao. Walipombeba wao walifikiri ana shida, yaani walimbeba kama kaomba lift au kama abiria. Yesu akija moyoni mwako haji kuomba lifti. Yesu ni Mtawala na huwezi kumuweka moyoni mwako kama abiria. Yesu sio Consultant ambaye unamtembelea siku una shida tu. Yaani unasema tutaonana tena katika Krismasi nyingine. Au tutaonana Jumapili nyingine nikija ibadani. Ukitaka mema mengi yakujie maana yake unatakiwa umjue Bwana. Na ukiendelea kukua kumjua Bwana basi uwe na uhakika ya kuwa kuna vitu atakuja na kumiliki ndani ya moyo wako. Ikiwa kuna vitu ambavyo hujamkabidhi Bwana na vinakutesa, na ukiendelea kukabidhi kwa Bwana basi Bwana atakusaidia na kuendelea kukupa vitu ambavyo haukuwa na utayari wa kubeba. Usikubali Yesu alale katika safari ya maisha yako ya mwaka 2024. Kama unasafiri katika safari ya mbali, au usiku huwa unamsemesha dereva ili asilale. Unapiga nae soga hizi na zile, sio kwamba una soga nyingi bali ni unataka asilale. Katika mwaka huu 2024 msemeshe Yesu ili asilale. Mweleze ushuhuda wako namna ambavyo Yesu kakusaidia katika maisha yako. Maana yeye ndio kiongozi wako, Yesu amehakikishwa naamini kuwa anaweza akakuongoza. Yesu atakuongoza katika maisha yako maana yeye ni Alfa na Omega. Sasa unaweza ukamuelewa Paulo aliposema bila Yesu ni hasara tu. Hata katika huduma Yesu akikuongoza kuna faida kubwa sana. Maana msalaba ni wa kwako binafsi maana ndio Yesu alikuokoa. Paulo alisema nimjue yeye na uwezo wa kufufuka kwake. Maana yake alipiga hesabu na akajua yote haya.  Mungu akubariki sana unapoenda kufuatilia semina hii. Ungana nasi katika maombi na sadaka. Bonyeza link pale juu ili uungane nasi.  🙏🙏🙏🙏🙏🙏🙏🙏🙏

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni