Jumatatu, 27 Februari 2023

DHAMBI NA MATAWI YAKE

Maana ya dhambi kiujumla ni uasi juu ya sheria au maagizo ya Bwana. Pia dhambi ni hali ya kupungukiwa au kutokuwa na upendo kwa Mungu. (Kumb 9:24 Mmekuwa na uasi juu ya Bwana tokea siku nilipowajua ninyi.) Najua baadhi tumeiskia maana hizi kama nilivyo fafanua kiufupi, lakini leo naomba kujaribu kuongezea kitu katika ufafanuzi wa ziada juu ya neno dhambi. Neno Dhambi linaweza kuwa neno kuu lenye vipengele kadhaa nimeviita matawi kama ifuatavyo:- VIPENGELE/MATAWI YA DHAMBI i. Makosa ii. Uasi iii. Uovu Baadhi ya watu wamekuwa wakimaanisha maana moja pale wanapotumia neno (dhambi)na neno (uovu) lakini kuna utofauti kidogo kati ya hayo maneno mawili, Tuanze kuangalia kiufupi tawi mojamoja tutapata jambo la kujifunza kama ifutavyo:- i. MAKOSA (Mwanzo 41:9,Basi mkuu wa wanyweshaji akamwambia Farao akisema, Nayakumbuka makosa yangu leo.) Huyu mnyweshaji ukichunguza kilichomponza ni kusahau. Katika tawi hili la dhambi mtu anaingia katika hatia dhidi ya sheria ya Mungu pasipo makusudio kamili ya Nafsi yake, (watu wengi huita bahati mbaya) Mfano:- unaweza kuwa katika kazi ya karani ukasaini malipo kwa vibarua sh300,000/= lakini ikatokea ukaongeza sifuri (typing error) ikawa wale vibarua wakachukua zao posho nene ya sh3000,000/= katika kesi hiyo mwizi atakuwa aliyeidhinisha na unaweza fukuzwa kazi hata kama nia yako haikuwa wizi. Au Kwa upande wa udereva makosa yanatokea sana mtoto kaachwa na wazazi gafla kavuka barabara dereva kagonga na alijitahidi kukwepa ila kamuumiza mtoto basi hiyo ni mistake au makosa. ii. UASI Anza kutafakari juu ya andiko hili (Kut 34:7mwenye kuwaonea huruma watu elfu elfu, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi; wala si mwenye kumhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe; mwenye kuwapatiliza watoto uovu wa baba zao, na wana wa wana wao pia, hata kizazi cha tatu na cha nne.) Katika tawi hili asilimia kubwa ya watu wanapotamka neno dhambi humaanisha UASI, UASI ni kitendo cha kutenda kinyume au kukataa kutekeleza agizo au sheria ya Mungu ukiwa na ufahamu juu ya ukiukaji wa maagizo. Ufahamu wa kukiuka unaupata kupitia dhamiri ya ndani, mashauri ya Roho wa Mungu, au Watu wanaokuzunguka. (Mwanzo 4:6,7-Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde. Bwana akamwambia Kaini, Kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana?) Ukiangalia hapa kaini anapata ushauri wa Roho wa Mungu juu ya hatua yake inayofuata kuwa ni mbaya ni Uasi lakini hashauriki, Kama vile baadhi ya watu wakiona hawezi kumtukana mtu hujipa ulevi wa makusudi ili kujihalalishia matusi hii hali huwa ni mbinu ya kupingana na dhamiri safi ya Roho wa Mungu ndani yao. Katika tawi hili haiangaliwi uzito wa Tukio la uasi kama kuua, kuiba, kudhalilisha au kuzini hapa msisitizo ni kuwa unachokifanya kiwe kina madhara mengi au machache ilimradi ulikifanya huku dhamiri ikikuhukumu kuwa unakiuka agizo huo ni UASI kwa Mungu. Mfano:- Sauli aliambiwa au watu, wanyama na mfalme yeye akamuacha mfalme akiwa hai na wanyama walonona . Kisa aliwaogopa askari wake Adhabu yake alifukuzwa kazi kwa KUASI agizo la Mungu makusudi. iii. UOVU Uovu ni nguvu ya mauti/uharibifu inayokuwa juu ya mtu fulani ikimshurutisha kutenda jambo lisilofaa mbele za Mungu na watu pasipo kuwa na uwezo wa kujizuia hata dhamiri yake inapomshuhudia kuwa kutenda jambo hilo ni vibaya , Hili ni tawi lingine la dhambi ambalo bado halijafafanuliwa na wengi na ukweli wa mambo linamchango mkubwa wa uharibifu miongoni mwa watu hata wanaoamini/waliookoka. > Ni uasi unaofanywa na mtu kwa shinikizo la nguvu za giza zinazotekeleza adhabu ya Mungu kwa mtu au familia kutokana na uasi wa watangulizi ndani familia,koo,jamii au taifa ( kama alivyosema Mungu napatiliza wana maovu ya baba zao) Mfano:- a} Ibrahimu alipotaka asiuawe alihimiza sara kuwa ni dada yake wakati huo Ibrahimu alifanya Uasi, ila Isaka pia na yeye alihimiza rebeka ni dada yake alifanya uovu wa baba yake.( hata kama ibrahimu alipiganiwa na Mungu kurejeshewa mke Isaka hakuweza kuamini kuwa atalindiwa mke na Mungu) b} Kaini aliua mtu yaani Habili alifanya Uasi ,tunamkuta mjukuu wake Lameki akijisifu kufanya Uovu wa kuuwa mtu(Mwanzo 4:23 Enyi wake za Lameki, sikilizeni usemi wangu; Maana nimemwua mtu kwa kunitia jeraha; Kijana kwa kunichubua;) c} Daudi aliasi sheria ya ndoa kwa kuzini na mke wa Uria na kama hiyo haitoshi akamwua na Uria pia alifanya Uasi, Jambo hilo likasababisha wanawe kufanya Uovu kutokana Uasi wa baba yao Daudi MATUKIO YA UOVU WA WANA WA DAUDI >Mtoto wa Daudi aitwaye Amnoni alimbaka Tamari Dada yake > Mtoto wa Daudi Absalom alimwua Amnoni kwa kisasi cha kubakwa dadaye wa tumbo moja > Absalom alimpindua kutoka katika ufalme Daudi babaye Yote hayo yalitokea baada ya Uasi wa sheria ya Ndoa kwa kuharibu Nyumba ya Uria na Mungu akapatiliza UOVU ulioharibu utawala na nyumba ya Daudi pamoja na Tabia za Watoto wake mbele ya macho yake Daudi. d} Au kuna baadhi ya watu walijitenga na madhehebu yao ya awali kwa hila ya ubinafsi waka ASI sheria ya Upendo wakaanzisha madhehebu mapya lakini baada ya muda fulani yanatokea matengano matengeno zaidi zaidi, watu hushangaa kwanini wanatengana kila mara, hapo shetani anakuwa kazini kisheria kwakuwa kanisa lilipewa sheria kuu ya upendo kwahiyo kujitenga kwaweza kuwa mwiba wa kudumu kwa ajitengaye. Huo ndio uovu unavyoleta uharibifu toka kizazi kimoja kwenda kingine Kule kujitenga inakuwa Tendo la Uovu . (kut 20:5 Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne. Katika eneo la Dhambi tawi la uovu kwa asilimia kubwa shetani hupata kibali cha kisheria kuishikilia familia, ukoo, kabila , taifa ili kutekeleza adhabu ya Mungu ya kupatiliza uovu ulotokana na UASI walofanya mababa wa familia, wakuu wa ukoo, wakuu wa taifa kwenda kwa kizazi kingine kwa namna ambayo kama watu hao hawakuipata neema ya Ukombozi kwa damu ya Yesu utawakuta wanateseka na Ugumu wa kuacha Dhambi hata kama hawapendi kutenda UOVU hivyo watakosa kuona Baraka za Bwana hata kama wameokoka. Mfano wa Koo mbali mbali nchini zilizoshikiliwa na nguvu ya uovu kwa muda mrefu. > Wapo walio na ulevi asilimia kubwa > Wapo waliowashirikina asilimia kubwa > Wapo waliowabishi asilimia kubwa > Wapo matapeli asilimia kubwa > Wapo malaya asilimia kubwa > Wapo wenye dharau na kiburi pia Uovu huo ukipevuka na kukomaa utamskia mtu miongoni mwao akisema yaani “ukinikosea utajua mimi natokea sehemu fulani sisi ukoo wetu huwa haturudi nyuma” ukisikia hivyo jua anazungumzia kuwa chanzo ni watangulizi Na Ukijaribu kumahauri miongoni mwao aache atakwambia tangu wazee wamefanya na mwingine atasema hata sijui naachaje maana nishajaribu nikashindwa, miungu ilishapata kibali cha kisheria ya kuwatesa na kuwadhibiti ili waendelee kutenda uovu wa dhambi walizotenda watangulizi wao PIA HALI HII UNAWEZA KUIITA MATATIZO YA KUIRITHI maana uovu ni suala la kiurithi ndiyo maana jambo ni la Baba wanaathirika ni watoto na wajukuu. HITIMISHO Nimetumia muda mwingi zaidi kufafanua kuhusu Uovu maana mtu aliyeokoka husumbuliwa sana na UOVU kwa sababu ni dhambi ya kiurithi na haiondolewi kwa mda mfupi bali Kwa kuzama kwanza katika Maarifa ya Utukufu wa Mungu ili ujue kona zote za kuutubia Uovu huo ili nguvu za Roho mtakatifu zikakufungie yaani kuyaondoa mapepo au miungu iliyoshikilia Hati ya mashitaka huko mahakama kuu ya mbinguni hivyo sheria ya Bwana ndiyo Uhuru wako na ukombozi wako na anasema mwenyewe ( KUT 20:6 Nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu.) Kumbuka alisema mkinipenda mtazishika sheria zangu ndo maana nikasema cha kwanza ni kuzama katika maarifa ya Ufalme wa Mungu ujue haki yako mbele zake Kristo aliye wakili mahakama kuu kwa ajili ya waliompokea. Amina Tafakari nami.......... MUNGU AKUBARIKI

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni