Alhamisi, 15 Februari 2024

SEMINA YA NENO LA MUNGU UWANJA WA RELI-ARUSHA: NA MWL. CHRISTOPHER  MWAKASEGE

SIKU YA PILI : 11 JANUARI, 2024 SOMO : MALENGO MKAKATI YA KUFANIKISHA MIPANGO YAKO LINK YA SOMO LA HILI YOUTUBE 👇🏼                                         https://www.youtube.com/live/aEiFAFxT__g8?si=odxQ9pqravFfCeGf  NAMBA ZA KUTUMA SADAKA, MAOMBI NA SHUHUDA 👇🏼  https://bit.ly/Sadaka-Maombi-Shuhuda  KUJIUNGA GROUP LA TELEGRAM: 👇🏼  https://t.me/Mwakasegemanaministry   UTANGULIZI  MALENGO YA SOMO Katika somo hili tuna malengo makubwa mawili. 1. Kukumbusha juu ya umuhimu wa malengo mkakati ya Kibiblia yaliyowekwa ili kubeba mipango kimafanikio. 2. Kukujulisha namna ya kugeuza lengo la kawaida kuwa lengo mkakati linalotekelezeka na linalofikika. Yerema 29:11 “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.” Katika tafsiri nyingine wamesema siku zenu za baadae lakini katika kiingereza wamesema Jeremiah 29:11 NIV “For I know the plans I have for you,” declares the Lord, “plans to prosper you and not to harm you, plans to give you hope and a future.” Ayubu 22:21 “Mjue sana Mungu, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia.” Kama mpango wako ni kumjua Mungu kwa mwaka huu unatakiwa kuweka mikakati ya kumjua Mungu mana ndio inakuja kubeba vingine vyote.  Ngoja tuone tofauti ya lengo mkakati na mpango mkakati: Watu wengi wana mipango na wana mikakati ya vitu vya kufanya bila malengo. Na kwa sababu hiyo ukiwauliza mwaka huu katika jambo wanalofanya wamekusudia kufika mpaka wapi, hawana jibu. Au mwingine atakuambia ni kwa kadri Mungu atakavyomwezesha.  Inaweza ikawa ni jibu lakini si jibu sahihi sana kwa sababu utaona hajui mahali ambapo Mungu amekusudia amfikishe.  MFANO: Ukiwa kwenye mpango wako wa kufanikiwa na ukafungua duka na ukaamua kuuza vitu hapo, lengo lako ni nini? Je! Ni kuuza vitu tu au kupata hela?  Kwa sababu kuna watu wanafurahia kwamba vitu vimeisha dukani bila kujua wamepata shilingi ngapi. Kwani ikifika mwisho wa mwaka atasema hajui kwa nini mtaji wake umekata. Hiyo ni kwa sababu hakuweka malengo ya kupata kitu kutoka kwenye duka hilo na umeenda hivyo miaka mingi bila kuwa na mafanikio kipesa.  Sasa kama Mungu amekupa lengo ndani yake ataweka na mkakati wa kukusaidia ili uweze kufikia lengo hilo. Na utakuja kujua kama umemjua Mungu kwa kiasi gani (kidogo, wastani au kikubwa). Itakuwa vigumu sana kujipima mwenyewe lakini ukishaanza kujifunza juu ya mikakati itakusaidia kwa namna ambayo itakuongezea kiu.  MIKAKATI YA KUMJUA MUNGU ILI IKUSAIDIE KUWEKA KATIKA MALENGO YAKO YA MWAKA HUU NA KATIKA MAISHA YAKO MKAKATI WA KWANZA FAHAMU KUNATOKEA NINI KWAKO UNAPOMJUA MUNGU Ufahamu utakuongezea kiu ya kumjua Mungu kwa kina zaidi bila kitu chochote kuingia katikati hapo kukukwamisha kutekeleza mkakati huo.  Wafilipi 3:7-10 “Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo; tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa imani; ili nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso yake, nikifananishwa na kufa kwake;” Tujiulize kwa nini amesema mambo yote amehesabu kuwa hasara?  Haina maana kwamba kila kitu alichofanya kilikuwa kibaya, bali amejisemesha mwenyewe kuwa hasara ya kitu anachokifanya haiwezi kubadilisha nafasi aliyompa Mungu maishani mwake. Hata kama anapata faida lakini Yesu akapoteza nafasi anayostahili, vitu vingine vyote ni hasara.  Kuna kitu amekiona kuhusu uzuri usio na kiasi wa kumjua Yesu Kristo Bwana wake.  Kuna uzuri fulani yeye ameuona na sisi wengine hatuuoni ingawa anajaribu kutueleza mpaka anaongea maneno mazito hayo.  Kwa tafsiri nyingine anamaanisha: “KUMJUA YESU KRISTO BWANA WAKE NI BORA ZAIDI KULIKO KUMTUMIKIA”  Kama kumtumikia Mungu kumechukua nafasi ya kwanza kuliko kumjua Yeye aliyekupa hiyo kazi, ujue kuna shida mahali. Kama faida na kufanikiwa kwako kutanyang`anya nafasi ya ushirika na Mungu.  Swali ambalo utakuwa unajiuliza kuwa ni kitu gani kinatokea unapomjua Mungu. Paulo alipata kitu kikubwa kuliko vitu vingine vyote. Leo tunatazama vitu ambavyo vinatokea ukimjua Mungu. KITU CHA KWANZA KUMJUA MUNGU KUNAKUBADILISHA WEWE NI NANI NDANI YAKO NA NJE YAKO Danieli 11:32b Lakini watu wamjuao Mungu wao watakuwa hodari, na kutenda mambo makuu. Hapa nataka uangalie sana lile neno, watu wamjuao Mungu watakuwa. Kabla hawajamjua Mungu hawakuwa. Knowing God changes you. Ukimjua Mungu inakubadilisha wewe ni nani, kunakubadilisha ndani. Watu wanakuwa hawana namna ya kukuuliza kuwa ni kitu gani kimetokea. Lakini watajua kwa nje maana utatenda mambo makuu. Hawatajua namna unavyotenda bali watajua unachotenda. Japo kuna wengine watataka kucopy namna unavyofanya lakini hawataweza kucopy unavyofanya. Maana unavyotenda inatokana na yule aliye ndani yako. Paulo alikuja kugundua kuwa anachofanya kinatokana na yule ambaye anamjua ambaye anataka awe kama anavyotaka, na ya kuwa anachofanya kitakuwa ni hasara tupu kama hamjui huyo ambaye anatakiwa kumbadilisha ndani ili awe anavyotaka awe ili sasa aweze kufanya kwa namna ambavyo anataka afanye ili apate matokeo ambayo anayataka.  Kwa hiyo kama hajambadilisha, hicho kitu anachokifanya ni hasara. Hii itakusaidia sana kila mara unapoingia katika maandiko na kusoma mstari wa kumjua Mungu. Fuatilia kitu gani kinatokea unapomjua Mungu. Kama hakijatokea kwako basi ujue bado hujamjua Mungu. Kuna picha Mungu alikuwa nayo alipotuleta Duniani, alitupa sura yake, mfumo wake, mamlaka yake na kitu cha kufanya. Dhambi ilipoingia ilitubadilisha tuliyokuwa na tukabadilika  tunavyofanya. Kwa hiyo ni lazima uokoke uwe kiumbe kipya, maana huwezi kusimama katika ile nafasi ambayo Mungu amekupa, maana kuna nafasi nyingine unapewa na msalaba na neema.  Huwezi ukamjua Mungu bila kumjua Kristo. Yesu alisema aliyeniona mimi amemuona baba.  Kazi inaweza kuwa ile ile unayoifanga lakini kadri unavyomjua Mungu mwaka huu kiwango chako kikiongezeka utendaji wako utabadilika kabisa. Hiki ni kitu kinatoka ndani, maana kiu ya kuona ufanisi unaongezeka inakuwa ni kiu yako ya ndani. Mtu wa ndani ndio anakuwa na vigezo vyake vya ufanisi, maana ndani yake ndiko Mungu kaweka viwango na vigezo vya ufanisi. Na huyo ndio ataamua kuwa hatuwezi kuendelea kwa staili hii. Je umewahi kuona nguo mpya zipo katika mitumba, maana yake kama umeona hizo nguo basi tambua ya kuwa zimekosa kiwango na ndio maana zipo hapo katika mitumba. Wewe unaweza usijue lakini kama hicho kitu kimekosa kiwango kinakuwa reject na kwenda katika mtumba au tabaka la chini kidogo. Huyu mtu ambaye Mungu anamtengeneza ndani yako kuna viwango Mungu anaweka. Sasa kuna watu ambao watapenda mtumba lakini wapo ambao watadaka na kufurahia viwango vipya. KITU CHA PILI KUMJUA MUNGU KUNABADILISHA VITU UNAVYOKUWA NAVYO NDANI YAKO NA NJE YAKO Ayubu 22:21** “Mjue sana Mungu, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia.” Kumjua Mungu kunaweka vitu ndani yako na kukubadilisha wewe. Biblia inasema kadri unavyozidi kumjua Mungu ndivyo amani inaongezeka. Isaya 9:6 “Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani.” Si tu kwamba Yesu anakubadilisha na kuwa mtu mwingine ila pia ataweka kitu cha kusaidiana naye ambayo mojawapo ni amani.  Kazi kubwa ya amani ni kutawala roho yako na maamuzi yako. Sasa watu wengi sana wakitaka kufanikiwa hawafuati mifumo ya kimafanikio. Mafanikio yako yanategemea nani yupo kwenye mifumo ndio maana watu wengi sana waliookoka wakiingia kwenye mifumo kiroho chao kinapoa kwa kutokumjua Mungu sana ili wawe na amani ambayo italinda maamuzi yao.  Wafilipi 4:6-7 “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.” Baada ya kuingia kwa dhambi duniani ukishaanza kufanikiwa shetani asingependa kuona watu wa Mungu wanaanza kufanikiwa na ndio malengo yake popote iwe kazini au ndani ya familia yako. Shetani anataka Mungu asipate heshima yake kwa kuonyesha kuwa ameshindwa kuwatetea watu wake.  Ukiomba Mungu akufanikishe atakupa maelekezo hiyo ni baada ya kuwa na amani inakupa utulivu na usikivu ndani yako.  sawa na  Isaya 1:19 “Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi;” Kwa hiyo lazima tuwe na kifungo cha amani na Mungu atatupa watu wa kushirikiana nao kila sehemu na katika miji mbalimbali na hata tunapoishi. Usichague wa kuambatana nao kwa kuwatazama. Unaweza kukwama kabisa.  Saa nyingine wengi wanachaguana kwa sababu ya kuokoka kwao.  Mfano mnachaguana kufanya biashara pamoja kwa sababu mmeokoka. Hicho kigezo hakitoshi.  Unaweza ukakuta ameokoka na hakuitiwa kufanya biashara kumbe ni mkulima kabisa sasa unajikuta wewe unabeba kila kitu.  Muda mwingine mkikaa kwenye kikao cha bodi mwanzo hadi mwisho hukuti akiwa na mchango zaidi ya kusema “NDIYO”. Akiulizwa labda ana neno lolote atasema “HAPANA, LAKINI FULANI UNAJUA AMETOA WAZO ZURI SANA MIMI NAFIKIRI TUKUBALIANE NAYE”. Mwisho wa mwaka anapokea gawio lake halafu unaanza kukosa amani bila kujua kakukosea nini. Muda mwingine watu wanakuwa waoga kufanya maamuzi sahihi na mambo yao mengi kukwama. Hiyo ni kwa sababu umembeba Yona wako kwenye boti lako. Utapata hasara tu kutokana na mengi kuharibika au umeyaacha njiani.  Muhimu sasa umjue Mungu sana ili vitu vya namna hii visitokee ili usikose mema yako.  Neno linaposema “NDIVYO MEMA YATAKAVYOKUJIA” humaanisha mtiririko wa mema kuja kwako kwa mfululizo. Yaani Mungu anakufungulia yote na si muujiza mmoja mmoja kwa muda mrefu.  MFANO: Fikiria kwa mwezi unapata TShs laki sita halafu sasa Mungu anakuambia kuanzia sasa kila siku nakupa TShs laki sita (TShs 600,000) sawasawa na Kumb. 28 : 1 - 14. Sasa nakuuliza Je! Moyo wako una uwezo wa kubeba hiyo laki sita?  Kwa sababu hizo baraka zimeamriwa kukufuata na kukupata.  Maana yake zitakufuata (ukijaribu kukwepa, umelala, umeamka, unafurahi, una hasira n.k.. zinakuja). Na watu wanaotumia nguvu za giza watasema wewe utakuwa mchawi sana kumbe wewe umemjua sana Mungu wako.  Muda mwingine ni rahisi sana kusema kikombe changu kinafurika (sawa, inaweza kuwa ni kipimo chako) unakuja kugundua watu wengine wanakuja kufaidi kuliko wewe kutokana na kibebeo chako kuwa ndogo. Sasa Mungu anakuja kukupa namna ya kuchukulia kipimo hicho.  Mungu anapokuja kwako anakuja kukuwekea utulivu na amani ya kupokea maelekezo anayokupa ili upate imani ya kufika kule alikokupangia.  JAMBO LA TATU LINALOTOKEA KWAKO UNAPOMJUA YESU KUMJUA MUNGU KUNAONGEZA UWEZA WA MOYO WAKO WA KUMBEBA YESU ALIVYO MOYONI MWAKO NA KWA AJILI YAKO Marko 4:35 - 41 “Siku ile kulipokuwa jioni, akawaambia, Na tuvuke mpaka ng’ambo. Wakauacha mkutano, wakamchukua vile vile alivyo katika chombo. Na vyombo vingine vilikuwako pamoja naye. Ikatokea dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji. Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia? Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu. Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado? Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?” Hawa watu hawakutakiwa wambebe Yesu kwenye boti tu bali wambebe na mioyoni mwao kwanza ndio wamwingize kwenye boti lao. Utajua hili baada ya wao kumwamsha na Yeye kuwauliza kuwa “HAWANA IMANI BADO?”  Kuna imani walitakiwa kuwa nayo kabla hawajakutana na dhoruba. Aliwaelewesha juu ya imani wanayopaswa kuwa nayo ila wakazoea yale mazingira ya bahari ya kutokuwa na mawimbi iwe mchana au usiku.  Ila sasa katika Marko 2: 1 - 12 utaona habari za mtu aliyepooza na watu kadhaa walimbeba ili aponywe na Yesu. Wakafungua dari na kumteremsha hadi alipo Yesu. Sasa Yesu alipoiona imani ya wale watu (si imani ya mgonjwa) akaachilia neno la uponyaji. Yesu aliona imani yao ikitoka mioyoni mwao na imani hiyo ikambeba mikononi mwao aliyepooza kwa hiyo moyo ndio uliokuwa umembeba aliyepooza. Moyo ulipombeba ukaelekeza mikono yao na hatua zao.  Kwenye Marko Yesu alipowauliza kuwa hawana imani bado ukilinganisha na hii hawa waliombeba aliyepooza unaona vitu viwili tofauti.  Ndipo Yesu akasema aliyepooza amesamehewa dhambi zake kwa sababu imani yao ilionekana mbele za Mungu.  Hata kama hujui kujieleza imani yako na matendo yako vitaonekana mbele za Mungu.  Wale wenye mashaka ndipo Yesu akawaambia kipi kigumu kwake? Kwa sababu anaweza kusamehe dhambi, ya aliyepooza akanyanyuka baada ya kuambiwa amesamehewa dhambi, akasimama na kuondoka.  Ndipo unakuja kuona swali la wanafunzi “Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?” Ukikata katikati hiyo sentensi utaona vitu viwili: 1. Imani yao kwa Yesu (Yesu ni nani kwao) [Ni nani huyu].  2. Imani inayosimama kwenye matendo [hata upepo na bahari humtii?].  Je Yesu alikuwa anatafuta imani gani? Maana ile kwamba wale watu wameacha kila kitu na wameamua kumfuata Yesu ina maana walikuwa na imani naye. Lakini swali la Yesu alikuwa alipouliza je hamna imani bado maana yake kuna imani nyingine ambayo alikuwa anaitafuta.  Hapa ina maananisha kuwa hawa watu walikuwa na imani ambayo katika mazingira yale ilikuwa haina msaada kwao. Ni muhimu sana uwe na imani ambayo inashughulika na mazingira yako uliyonayo.  Hili swali Yesu aliwauliza kuwa je watu huko mtaani wanasema mimi ni nani?  Na je nyie mnasema mimi ni nani? Walimuona Yesu ng’ambo ya pili akikemea pepo lakini wameingia katika boti hawamjui tena huyu Yesu. Kwa hiyo hawakuweza kumuamini. Ukimjua Mungu anakuja ndani ya moyo wako. Ndani ya moyo wako dhambi ilipoingia, ilimuondoa Yesu na ikapunguza vitu vingine. Lakini sasa ukianza kumjua Yesu ile imani ndani yako kuna vitu inaanza kuingiza ya kumjua yeye ni nani. Kwa hiyo hali ya namna hiyo itaanza kudai nafasi. Sasa Yesu alipowauliza swali wanafunzi wake mbona mmekuwa waoga, ina maana kuna mahali imani yao ilitakiwa ikae katika nafasi kama hiyo lakini haikukaa na inaonesha kulikuwa na kitu kingine pale. Je katika mazingira ya mwaka 2024 Yesu ni nani kwako.  Kama kuna mahali unapita na mahali unapopita ni papya, unajikuta unapata hofu. Tunakuuliza kwa nini unakuwa mwoga unasema  Yesu ninaye. Lakini kwa kweli kuna imani ulitakiwa uwe nayo na sasa hauna. Ni kwa sababu hujamjua Yesu kuwa ni nani katika eneo hilo. Yesu anaingia ndani yako na kufanya uwe na imani maalumu yaani ya kumbeba moyoni mwako. Wale wanafunzi walikuwa wamembeba Yesu katika chombo na hawakumbeba moyoni mwao. Maana wangembeba moyoni mwao wasingekuwa na hofu. Amani ambayo Mungu anakupa haijalishi yapo mawimbi kama yapo au hayapo bado unakuwa na amani ndani yako. Ndani yako kukijaa Kristo ambaye unamjua unakuwa hauna hofu. Yesu aliingia katika boti na uwezo wake aliokua nao ulikuwa ni kwa ajili yao. Walipombeba wao walifikiri ana shida, yaani walimbeba kama kaomba lift au kama abiria. Yesu akija moyoni mwako haji kuomba lifti. Yesu ni Mtawala na huwezi kumuweka moyoni mwako kama abiria. Yesu sio Consultant ambaye unamtembelea siku una shida tu. Yaani unasema tutaonana tena katika Krismasi nyingine. Au tutaonana Jumapili nyingine nikija ibadani. Ukitaka mema mengi yakujie maana yake unatakiwa umjue Bwana. Na ukiendelea kukua kumjua Bwana basi uwe na uhakika ya kuwa kuna vitu atakuja na kumiliki ndani ya moyo wako. Ikiwa kuna vitu ambavyo hujamkabidhi Bwana na vinakutesa, na ukiendelea kukabidhi kwa Bwana basi Bwana atakusaidia na kuendelea kukupa vitu ambavyo haukuwa na utayari wa kubeba. Usikubali Yesu alale katika safari ya maisha yako ya mwaka 2024. Kama unasafiri katika safari ya mbali, au usiku huwa unamsemesha dereva ili asilale. Unapiga nae soga hizi na zile, sio kwamba una soga nyingi bali ni unataka asilale. Katika mwaka huu 2024 msemeshe Yesu ili asilale. Mweleze ushuhuda wako namna ambavyo Yesu kakusaidia katika maisha yako. Maana yeye ndio kiongozi wako, Yesu amehakikishwa naamini kuwa anaweza akakuongoza. Yesu atakuongoza katika maisha yako maana yeye ni Alfa na Omega. Sasa unaweza ukamuelewa Paulo aliposema bila Yesu ni hasara tu. Hata katika huduma Yesu akikuongoza kuna faida kubwa sana. Maana msalaba ni wa kwako binafsi maana ndio Yesu alikuokoa. Paulo alisema nimjue yeye na uwezo wa kufufuka kwake. Maana yake alipiga hesabu na akajua yote haya.  Mungu akubariki sana unapoenda kufuatilia semina hii. Ungana nasi katika maombi na sadaka. Bonyeza link pale juu ili uungane nasi.  🙏🙏🙏🙏🙏🙏🙏🙏🙏

JIFUNZE KUTOPUUZIA MAMBO MADOGO NA KUTOCHUKULIA KAWAIDA MAKOSA MADOGO MADOGO

JIFUNZE KUTOPUUZIA MAMBO MADOGO NA KUTOCHUKULIA KAWAIDA MAKOSA MADOGO MADOGO Mfano imetokea nimelala mpaka asubuhi bila kuamka na kufanya maombi, isichukulie kawaida. Usipuuzie. Inatakiwa moyoni uumie na kujiuliza, Ni Kwanini sijaamka kuomba ?! Inamaana nimeshindwa kuwa na muda na Mungu hata kwa muda mfupi Usiku mzima ?! Yesu hakuchukulia kawaida kwa akina Petro kushindwa kuomba pamoja naye usiku ule, akawaamsha na kuwauliza, hamkuweza kukesha hata saa moja ?! HATA KAMA WATU WENGINE WATACHUKULIA KAWAIDA LAKINI WEWE USIPUUZIE WALA KUONA NI KAWAIDA, SHITUKA Imetokea Siku nzima inapita sijapata muda wa KUSOMA BIBLIA, Au nimeamka na kuendelea na majukumu yangu bila KUMSHUKURU MUNGU KWA KUNIAMSHA SALAMA. Au nimesinzia bila kusali usiku KUJIKABIDHI KWA MUNGU. Au siku nzima inapita sikupata muda wowote wa kuongea na Mungu kwa Sala na maombi. Kamwe usipuuzie au kuchukulia kawaida makosa madogo madogo ya aina hiyo, usikubali uongo ambao adui anakwambia eti ulikuwa bize hata Mungu anajua. Ukweli ni kwamba, wakati mwingine unasumbuka na mambo mengi wakati unaliacha FUNGU LILILO JEMA AMBALO HALIPOTEI, Jiulize, kwa nini hata kama uko bize kiasi gani, lazima uwe na muda wa kula, hata uwe bize kiasi gani, lazima baadaye utapumzika au utalala usingizi hata kama ni kwa kuchelewa, hata uwe bize kiasi gani, lakini asubuhi unapoamka unapata muda wa kuvaa nguo, kupiga mswaki n.k Kama pamoja na ubize wote ulionao, bado kuna mambo hautaacha kuyafanya ili uendelee kuonekana nadhifu na pia ubaki na nguvu za kuendelea kufanya kazi, Unakosaje ratiba muhimu ili roho yako iendelee kuwa na afya pia Mungu aendelee kukutetea ?! Kwa nini usitumie dakika kadhaa kabla ya kula, kulala, kuvaa nguo, kuoga n.k ukaanza kuomba au kusoma biblia kisha ukaendelea na ratiba zako ?! KINACHOKUZUIA SIO UBIZE, BALI NI KUTOONA UMUHIMU WA NENO NA MAOMBI KWENYE MAISHA YAKO. CHOCHOTE AMBACHO UNAJUA KINA UMUHIMU KWENYE MAISHA YAKO LAZIMA UTAKIPA NAFASI KWENYE RATIBA ZAKO ZA UBIZE, KADHALIKA NA YESU AKIWA NA UMUHIMU KWAKO, LAZIMA UTATAFUTA MUDA WA KUONGEA NAYE. Tabia ya kupuuzia au kuchukulia kawaida makosa madogo madogo, baada ya muda huwa inakomaa na kuwa tabia halisi. Yaani inakuwa ni tabia yako Kulala bila kusali, kuamka bila KUMSHUKURU MUNGU, Inakuwa ni tabia yako kutokusoma Neno la Mungu na kutofanya maombi. Wengine tayari wameshakuwa na tabia hata ya kutosali Jumapili au kuhudhuria vipindi vya katikati ya wiki, Mungu atusaidie sana. Inapaswa nianze kuwa na mtazamo kwamba, nisipofanya yale ninayopaswa kufanya nijihisi kama nimemkosea Mungu, natakiwa nirudi mbele za Mungu kuomba toba. Nimwambie Mungu nimekuwa mzembe naomba unisamehe. UJUE KUNA MAISHA UKIYAISHI DHAMBI INAKUWA HADITHI KWAKO UTAKUWA UNAISIKIA KWA WATU WENGINE TU Sasa Wengi hawajui Kuwa kupuuzia makosa madogo madogo Huwa inaleta mazoea Hatimaye inakomaa inakuwa Ndiyo tabia ,na ikashakua tabia ni ngumu Sana kuja kujirekebisha Sababu inakuwa imeshaota mizizi. Hata watu walioanguka kwenye dhambi, nao walianza kwa kupuuzia mambo madogo madogo, kadhalika hata Samsoni alikamatwa baada ya kuchukulia kawaida maneno ya Delila akiona kama ni utani, kumbe alikuwa ametumwa kwa lengo la kumdhoofisha ili adui wamkamate. Kama unataka kufika viwango Vya Juu Kiroho Moja kati ya Jambo ambalo unapaswa kulizingatia basi ni hili Epuka kuyapuuzia makosa madogo madogo na kuyachukulia Kawaida Kabisa Hata kama wengine wanachukulia Kawaida lakini wewe usiyachukulie Kawaida Unapogundua Kuna kosa lolote umelifanya usilipuuzie lilekebishe chapchap Unapogundua Kuna Mahali haupo sawa mfano umepunguza viwango Vya Maombi ,kusoma Neno , umepunguza Muda Wako na Mungu usipuuzie rekebisha haraka Sana kabla halijageuka Kuwa mazoea halafu Kuwa tabia Jifunze hili Kama unataka Kufika mbali Kiroho Maana mambo ya Kiroho yanahitaji NIDHAMU KUBWA SANA HAYATAKI MCHEZO MCHEZO ,HAYATAKI MASIHARA MASIHARA BARIKIWA KWA UJUMBE HUU.

Jumapili, 5 Machi 2023

IMANI YA KIMUNGU

(Ebrania 11:1-) Imani ya Kimungu ni kuwa na uhakika wa mambo unayoyatarajia kutoka kwa Mungu, ni bayana ya mambo yasiyoonekana. AU Imani ni kuwa na uhakika wa mambo unayoyatarajia kutoka kwa Mungu, Ni bayana ya mambo uliyoyaumba/yaliyoumbwa ulimwengu wa roho kwa neno lako au kwa neno la Mungu kabla mambo hayo hayajatokea au kudhihirika kwa macho ya kawaida. Kwa Imani twafahamu ya kuwa Ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu., na Vitu vinavyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo dhahiri/vinavyoonekana. HATUA ZA MSINGI KUJENGA IMANI i. Kuwa na Wazo (luka 12:17) ii. Kulitafakari/kulimeng’enya iii. Kupata uhakika kuwa wazo ni sahihi/kuwa na msimamo/ kuwa na amani ya Kristo. iv. Kulikiri kwa kinywa mbele za Mungu kwanza na kwa watu wanakuhusu. Kwa mfano, Mbunifu wa Majengo huumba/hubuni nyumba akilini mwake kabla yakuanza kuleta matofali na mawe Hutazama mwisho kwanza ndipo huanza kujenga (Isaya 46:10 nitangazaye mwisho tangu mwanzo,) Katika Imani ya Kimungu , Atoaye wazo sahihi ni Roho wa Mungu moyoni mwa mtu kupitia NENO LA KRISTO ambalo ni mbegu/wazo Baada ya kulichakata moyoni na nafsini hufuatia hatua ya kulipeleka kwa Mungu ili liumbike ulimwengu wa roho, ili kupitia nguvu ya IMANI ya mtu alivute au alikokote jambo hilo litokee katika ulimwengu wa Mwili kwa majira yake sahihi. i. Lipo linatokea papo kwa papo (Luka 4:35) ii. Lipo linatokea kwa masaa (Ebrania 11:17) iii. Lipo linalotokea kwa miezi na miaka (Isaya 7:14) Katika Imani ya kimungu kuna namna mbili za Imani :- i. Imani ya kupokea vitu vilivyokinyume na kanuni za kimwili au kijografia kama ilivyotokea kwa baadhi ya watu wa Mungu . Mfano:- .Joshua kusimamisha Jua/Dunia .Kukaushwa bahari ya shamu .Bikira kuzaa mwana .Yesu kufufuka kati ya wafu Katika Imani hii kuna nyenzo ya ziada ambayo ni Karama ya Imani kukusaidia katika kukamilika kwake. (1korinto 12:9 mwingine imani katika Roho yeye yule;) Omba karama ya Imani kama unamalengo yaliyojuu ya akili ya kibinadamu. ii. Imani ya kupokea vitu vya kawaida Kupona magonjwa, kufanikiwa kiuchumi, kupata mme/mke, kuongezwa cheo nk. Haya yote nimeyaweka katika kundi la Imani ya kawaida kwa sababu ni mwaliko wa kiujumla kwa kila aaminiye kama ilivyoandikwa “mwenye haki ataishi kwa Imani”(Ebrania10:38) KILA ALIYE NDANI YA KRISTO ANAYO IMANI. Kristo ndiye Mwanzilishi wa Imani yetu hivyo ameweka imani ndani yetu kupitia Roho wake anayetufundisha neno la Mungu kila siku. Swali:- Kama nina Imani kwanini ninamengi niliyoomba sijapokea? KWANINI SIPOKEI NILICHOOMBA KWA MUNGU i. Wazo lisilo na maslahi na Mungu , kwa mfano unatakuoa/kuolewa alafu unasema nataka mke wangu au mme awe na kazi fulani na mshahara fulani, ukikosa ulichoomba usilaumu mtu jilaumu wewe, n.k ii. Uoga , mara zote Yesu amewaonya wanafunzi akisema msiogope, uoga kwa watu wa Afrika ni mkubwa sana kiasi kwamba wanyama kama paka na bundi bado wana mamlaka mioyoni mwa watu. iii. Kuongea kinyume na ulichoumba kwa maombi . Mfano. Nchi hii kufanikiwa ni vigumu sana alafu jana usiku uliomba upate mtaji/kazi au unasema ninaumwa kaugonjwa ketu ila jana uliomba uponyaji, Utaishia kuomba bila majibu miaka yote. JIFUNZE HATUA HIZI UTAMWONA MUNGU MACHONI PIA 1. Wazo/neno la Mungu moyoni mwa mtu:- Nataka kupona ugonjwa neno msingi (Math 8:17 aliuchukua udhaifu wetu Na kuyachukua magonjwa yetu.) 2. Kutafakari neno au wazo hilo moyoni na akilini kuona Upendo na Huruma ya Mungu katika kukuponya (Luka 2:35 ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi) 3. Kuomba au kuwasilisha kwa Mungu akamilishe nia yake ya kuwaponya watu (Yohana 10:10 mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele) 4. Kubadili mtazamo usikione unachoona machoni yaani ule ugonjwa, badala yake ona kile kilichopo ulimwengu wa roho yaani uponyaji/uzima. katika hili hakusaidii mtu mwingine hata mtumishi wa Mungu ni wewe binafsi 5. Kiri kushinda wakati wote hata kama wanakucheka kuwa umechanganyikiwa kwa kusema kitu wasichokiona wenzako na adui wa Imani yako mkubwa ni yule mnayeheshimiana anaweza kuwa mtumishi pia , ukiwashinda wakatisha tamaa unaowaheshimu, basi Mungu hana kizuizi cha kudhihirisha/kuprinti kilichokuwa rohoni kuja mwilini, ndipo utasikia pongezi kwa wale wakatisha tamaa. MUNGU AKUBARIKI KATIKA TAFAKARI HII YA NENO LAKE

Jumatatu, 27 Februari 2023

DHAMBI NA MATAWI YAKE

Maana ya dhambi kiujumla ni uasi juu ya sheria au maagizo ya Bwana. Pia dhambi ni hali ya kupungukiwa au kutokuwa na upendo kwa Mungu. (Kumb 9:24 Mmekuwa na uasi juu ya Bwana tokea siku nilipowajua ninyi.) Najua baadhi tumeiskia maana hizi kama nilivyo fafanua kiufupi, lakini leo naomba kujaribu kuongezea kitu katika ufafanuzi wa ziada juu ya neno dhambi. Neno Dhambi linaweza kuwa neno kuu lenye vipengele kadhaa nimeviita matawi kama ifuatavyo:- VIPENGELE/MATAWI YA DHAMBI i. Makosa ii. Uasi iii. Uovu Baadhi ya watu wamekuwa wakimaanisha maana moja pale wanapotumia neno (dhambi)na neno (uovu) lakini kuna utofauti kidogo kati ya hayo maneno mawili, Tuanze kuangalia kiufupi tawi mojamoja tutapata jambo la kujifunza kama ifutavyo:- i. MAKOSA (Mwanzo 41:9,Basi mkuu wa wanyweshaji akamwambia Farao akisema, Nayakumbuka makosa yangu leo.) Huyu mnyweshaji ukichunguza kilichomponza ni kusahau. Katika tawi hili la dhambi mtu anaingia katika hatia dhidi ya sheria ya Mungu pasipo makusudio kamili ya Nafsi yake, (watu wengi huita bahati mbaya) Mfano:- unaweza kuwa katika kazi ya karani ukasaini malipo kwa vibarua sh300,000/= lakini ikatokea ukaongeza sifuri (typing error) ikawa wale vibarua wakachukua zao posho nene ya sh3000,000/= katika kesi hiyo mwizi atakuwa aliyeidhinisha na unaweza fukuzwa kazi hata kama nia yako haikuwa wizi. Au Kwa upande wa udereva makosa yanatokea sana mtoto kaachwa na wazazi gafla kavuka barabara dereva kagonga na alijitahidi kukwepa ila kamuumiza mtoto basi hiyo ni mistake au makosa. ii. UASI Anza kutafakari juu ya andiko hili (Kut 34:7mwenye kuwaonea huruma watu elfu elfu, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi; wala si mwenye kumhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe; mwenye kuwapatiliza watoto uovu wa baba zao, na wana wa wana wao pia, hata kizazi cha tatu na cha nne.) Katika tawi hili asilimia kubwa ya watu wanapotamka neno dhambi humaanisha UASI, UASI ni kitendo cha kutenda kinyume au kukataa kutekeleza agizo au sheria ya Mungu ukiwa na ufahamu juu ya ukiukaji wa maagizo. Ufahamu wa kukiuka unaupata kupitia dhamiri ya ndani, mashauri ya Roho wa Mungu, au Watu wanaokuzunguka. (Mwanzo 4:6,7-Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde. Bwana akamwambia Kaini, Kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana?) Ukiangalia hapa kaini anapata ushauri wa Roho wa Mungu juu ya hatua yake inayofuata kuwa ni mbaya ni Uasi lakini hashauriki, Kama vile baadhi ya watu wakiona hawezi kumtukana mtu hujipa ulevi wa makusudi ili kujihalalishia matusi hii hali huwa ni mbinu ya kupingana na dhamiri safi ya Roho wa Mungu ndani yao. Katika tawi hili haiangaliwi uzito wa Tukio la uasi kama kuua, kuiba, kudhalilisha au kuzini hapa msisitizo ni kuwa unachokifanya kiwe kina madhara mengi au machache ilimradi ulikifanya huku dhamiri ikikuhukumu kuwa unakiuka agizo huo ni UASI kwa Mungu. Mfano:- Sauli aliambiwa au watu, wanyama na mfalme yeye akamuacha mfalme akiwa hai na wanyama walonona . Kisa aliwaogopa askari wake Adhabu yake alifukuzwa kazi kwa KUASI agizo la Mungu makusudi. iii. UOVU Uovu ni nguvu ya mauti/uharibifu inayokuwa juu ya mtu fulani ikimshurutisha kutenda jambo lisilofaa mbele za Mungu na watu pasipo kuwa na uwezo wa kujizuia hata dhamiri yake inapomshuhudia kuwa kutenda jambo hilo ni vibaya , Hili ni tawi lingine la dhambi ambalo bado halijafafanuliwa na wengi na ukweli wa mambo linamchango mkubwa wa uharibifu miongoni mwa watu hata wanaoamini/waliookoka. > Ni uasi unaofanywa na mtu kwa shinikizo la nguvu za giza zinazotekeleza adhabu ya Mungu kwa mtu au familia kutokana na uasi wa watangulizi ndani familia,koo,jamii au taifa ( kama alivyosema Mungu napatiliza wana maovu ya baba zao) Mfano:- a} Ibrahimu alipotaka asiuawe alihimiza sara kuwa ni dada yake wakati huo Ibrahimu alifanya Uasi, ila Isaka pia na yeye alihimiza rebeka ni dada yake alifanya uovu wa baba yake.( hata kama ibrahimu alipiganiwa na Mungu kurejeshewa mke Isaka hakuweza kuamini kuwa atalindiwa mke na Mungu) b} Kaini aliua mtu yaani Habili alifanya Uasi ,tunamkuta mjukuu wake Lameki akijisifu kufanya Uovu wa kuuwa mtu(Mwanzo 4:23 Enyi wake za Lameki, sikilizeni usemi wangu; Maana nimemwua mtu kwa kunitia jeraha; Kijana kwa kunichubua;) c} Daudi aliasi sheria ya ndoa kwa kuzini na mke wa Uria na kama hiyo haitoshi akamwua na Uria pia alifanya Uasi, Jambo hilo likasababisha wanawe kufanya Uovu kutokana Uasi wa baba yao Daudi MATUKIO YA UOVU WA WANA WA DAUDI >Mtoto wa Daudi aitwaye Amnoni alimbaka Tamari Dada yake > Mtoto wa Daudi Absalom alimwua Amnoni kwa kisasi cha kubakwa dadaye wa tumbo moja > Absalom alimpindua kutoka katika ufalme Daudi babaye Yote hayo yalitokea baada ya Uasi wa sheria ya Ndoa kwa kuharibu Nyumba ya Uria na Mungu akapatiliza UOVU ulioharibu utawala na nyumba ya Daudi pamoja na Tabia za Watoto wake mbele ya macho yake Daudi. d} Au kuna baadhi ya watu walijitenga na madhehebu yao ya awali kwa hila ya ubinafsi waka ASI sheria ya Upendo wakaanzisha madhehebu mapya lakini baada ya muda fulani yanatokea matengano matengeno zaidi zaidi, watu hushangaa kwanini wanatengana kila mara, hapo shetani anakuwa kazini kisheria kwakuwa kanisa lilipewa sheria kuu ya upendo kwahiyo kujitenga kwaweza kuwa mwiba wa kudumu kwa ajitengaye. Huo ndio uovu unavyoleta uharibifu toka kizazi kimoja kwenda kingine Kule kujitenga inakuwa Tendo la Uovu . (kut 20:5 Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne. Katika eneo la Dhambi tawi la uovu kwa asilimia kubwa shetani hupata kibali cha kisheria kuishikilia familia, ukoo, kabila , taifa ili kutekeleza adhabu ya Mungu ya kupatiliza uovu ulotokana na UASI walofanya mababa wa familia, wakuu wa ukoo, wakuu wa taifa kwenda kwa kizazi kingine kwa namna ambayo kama watu hao hawakuipata neema ya Ukombozi kwa damu ya Yesu utawakuta wanateseka na Ugumu wa kuacha Dhambi hata kama hawapendi kutenda UOVU hivyo watakosa kuona Baraka za Bwana hata kama wameokoka. Mfano wa Koo mbali mbali nchini zilizoshikiliwa na nguvu ya uovu kwa muda mrefu. > Wapo walio na ulevi asilimia kubwa > Wapo waliowashirikina asilimia kubwa > Wapo waliowabishi asilimia kubwa > Wapo matapeli asilimia kubwa > Wapo malaya asilimia kubwa > Wapo wenye dharau na kiburi pia Uovu huo ukipevuka na kukomaa utamskia mtu miongoni mwao akisema yaani “ukinikosea utajua mimi natokea sehemu fulani sisi ukoo wetu huwa haturudi nyuma” ukisikia hivyo jua anazungumzia kuwa chanzo ni watangulizi Na Ukijaribu kumahauri miongoni mwao aache atakwambia tangu wazee wamefanya na mwingine atasema hata sijui naachaje maana nishajaribu nikashindwa, miungu ilishapata kibali cha kisheria ya kuwatesa na kuwadhibiti ili waendelee kutenda uovu wa dhambi walizotenda watangulizi wao PIA HALI HII UNAWEZA KUIITA MATATIZO YA KUIRITHI maana uovu ni suala la kiurithi ndiyo maana jambo ni la Baba wanaathirika ni watoto na wajukuu. HITIMISHO Nimetumia muda mwingi zaidi kufafanua kuhusu Uovu maana mtu aliyeokoka husumbuliwa sana na UOVU kwa sababu ni dhambi ya kiurithi na haiondolewi kwa mda mfupi bali Kwa kuzama kwanza katika Maarifa ya Utukufu wa Mungu ili ujue kona zote za kuutubia Uovu huo ili nguvu za Roho mtakatifu zikakufungie yaani kuyaondoa mapepo au miungu iliyoshikilia Hati ya mashitaka huko mahakama kuu ya mbinguni hivyo sheria ya Bwana ndiyo Uhuru wako na ukombozi wako na anasema mwenyewe ( KUT 20:6 Nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu.) Kumbuka alisema mkinipenda mtazishika sheria zangu ndo maana nikasema cha kwanza ni kuzama katika maarifa ya Ufalme wa Mungu ujue haki yako mbele zake Kristo aliye wakili mahakama kuu kwa ajili ya waliompokea. Amina Tafakari nami.......... MUNGU AKUBARIKI

Jumatano, 4 Machi 2020

DAMU YA YESU KRISTO

YOHANA 1:29

TAZAMA MWANAKONDOO WA MUNGU AICHUKUAE DHAMBI YA ULIMWENGU.
   " KWAKUWA TORATI ILITOLEWA KWA MKONO WA MUSA, NEEMA NA KWELI ZILIKUJA KWA MKONO WA YESU KRISTO   -YOHANA1:17"

 Ndugu katika Kristo Yesu ni Vema kuchagua kujua Umuhimu wa Sadaka ya Mungu yaani Yesu Kristo Mwanakondoo asiye na mapungufu wala dhambi,
Katika agano la Kale zilitumika Sadaka za wanyama kuleta upatanisho kati ya Mungu na Mwanadamu.
Katika agano jipya yaani Mungu amemwachilia mwanaye wa pekee Yesu Kristo awe Sadaka( yaani kafara) Takatifu
   UFUNUO 5:9(KWA KUWA ULICHINJWA UKAMNUNULIA MUNGU KWA DAMU YAKO WATU WAKILA KABILA NA LUGHA NA JAMAA NA TAIFA)..

   1.Ni vema kuamini Kifo cha Yesu kimerejesha mahusiano kati ya Mungu na Mwanadamu wa kila ukoo,kabila na taifa
   2. Ni vema kujua na kuamini kuitumia Damu ya Yesu kujitakasa Toka maisha machafu ya dhambi.
   3.Ni vema kuamini kuwa wanaotumia Damu za wanyama wako nje ya agano la Yesu wanatenda dhambi na wanaalikwa kuitumia Damu ya Yesu Wapate Utakaso na Kibali.

 DAMU YA YESU ILIYOMWAGIKA MSALABANI KWA AJILI YA WENGI KUWAONDOLEA DHAMBI

KAMA INAVYOFAFANULIWA

 (WARUMI 5:19-kwa sababu kama kwa kuasi kwake mtu  mmoja {Adamu} watu wengi waliingizwa katika dhambi,kadhalika kwa kutii kwake mmjo{Kristo} watu wengi wameingizwa katika hali ya
 haki)
""Hivyo Haki Hupatikana katika Kristo aliyefanyika dhambi ili wengi{watu} wapate Haki kwa Njia ya Msamaha""

Jumamosi, 22 Februari 2020

UPENDO WA KWELI

YOHANA 5:42(UPENDO)
"WALAKINI NIMEJUA NINYI HAMNA UPENDO WA MUNGU NDANI YENU"
BAADHI YA WATU WANAFAHAMU KUWA MUNGU NDIYE CHANZO CHA UPENDO''

KATIKA DUNIA HII NIMEGUNDUA NENO "UPENDO/LOVE" NI MAARUFU SANA
MF:-NI JADI KUSIKIA NENO 'KUPENDA' KATIKA MUZIKI NA FILAMU...
NIKAWA NAJIULIZA MASWALI....!
-Kama nyimbo nyingi zinazungumzia kupenda inamaanisha watu/Vijana wanaishi tabia ya Mungu ya UPENDO...?
-Pia nikajiuliza UPENDO tunaousikia katika  Muziki na filamu   ndo ule  wa kibiblia...?

BAADA YA KUJIFUNZA KATIKA NENO JUU YA KUPENDA NA UPENDO NIKAPATA KUISIKITIA JAMII YETU...pale ambapo inawategemea baadhi ya wasanii(makahaba) kama walimu wao wa upendo  ambao hata wao wenyewe wanahitaji kwenda darasani(Katika NENO) kujifunza UPENDO wa Kweli utakao watua katika  Mizigo ya migogoro ya nafsi ndani yao.

MITHAL 6:26(Na kahaba Humwinda mtu  anase nafsi yake iliyo ya thamani).

Kama wakristo waimbavyo katika  Ibada na kuufurahia uwepo wa Mungu ushukapo

Naamini ndivyo wanaokusanyika na baadhi ya wasanii makahaba wanavyokuwa wanafurahia uwepo wa malikia wao makahaba Yezebeli

-KAMA MWALIMU WAKO WA KUPENDA HAJUI HATA IDADI YA WENZA WAKE, MWANAFUNZI UTAKUW SALAMA..!!
-KAMA MWALIMU WAKO WAKO WA KUPENDA AMESHASAHAU KAMA KUNA WAZAZI NA WAKUBWA MWANAFUNZI UTAKUWA SALAMA..!!


WAEFESO 5:19(mkisemezana kwa Zaburi,na Tenzi na Nyimbo za Rohoni, Huku mkiimba na kumshukuru Bwana mioyoni mwenu)

UPENDO HAKIKA HAUTOKI MDOMONI BALI NI MATOKEO YA NEEMA YA MUNGU ILIYOMO NDANI YA AAMINIYE MATESO,KIFO NA UFUFUKO WA MWOKOZI YESU MWALIMU WA UPENDO WA KWELI (yohana 15:9)

Redio yako,simu yako,Tv yako,pc yako  hazitahukumiwa kwa kupitisha sauti ama video za kutomtukuza Mwenye Enzi Mungu Bali wewe uliyevitumia Vibaya.

SALA:- "Mungu Roho Mtakatifu Niongoze ili niwe na uchaguzi mzuri  juu ya yote ninayo angalia na kusikiliza" Amina.
Ubarikiwe Na Mungu Mtakatifu.

Jumatano, 19 Februari 2020

MKRISTO ANAANGUKAJE KATIKA ZINAA -Somo na Mwl. CHRISTOPHER MWAKASEGE


MKRISTO ANAANGUKAJE KATIKA ZINAA? (Somo na Mwl. Christopher Mwakasege)


          Kila mara nilipopata habari za watu wa Mungu walioanguka katika dhambi ya zinaa nilikuwa najikuta najiuliza swali hili, “Hivi wanapataje ujasiri wa kutenda tendo hilo?”

          Akili yangu ilikuwa inakataa kabisa kuamini kuwa mtu aliyeokoka (na wakati mwingine amejazwa Roho Mtakatifu) anaweza kuanguka kwenye dhambi ya zinaa. Lakini hata hivyo bado nikawa naendelea kusikia majina ninayoyafahamu ya watu wa Mungu waliookoka waliokubwa na dhambi ya zinaa.

“Wanafanyaje mpaka wanaanguka katika zinaa”? Hili swali lilinisumbua kwa muda mrefu. Na siku moja nilikuwa nyumbani kwangu nikijiuliza swali hili moyoni, nikasikia Roho Mtakatifu akiniuliza ndani ya moyo wangu, akisema, “ Kwani Daudi aliangukaje? Je! Umesahau ya kuwa naye alikuwa mtu wangu, mtumishi wangu niliyempaka mafuta?

          Niliposikia swali hili, nilichukua biblia na kusoma maneno yanayoeleza kuanguka kwa Mfalme Daudi katika dhambi ya zinaa na mke wa mmoja wa askari wake.

          Mambo niliyoyasoma yalinifungua macho kuona jinsi ambavyo hata hivi leo watu wa Mungu wanavyoanguka au wanavyoweza kuanguka katika dhambi ya zinaa.

          Chukua biblia yako na usome habari hizi katika 2 Samweli 11:1-27 na 2 Samweli 12:1-25.

          Chanzo cha kuanguka kwa Mfalme Daudi katika dhambi ya Zinaa, ni KUTOKWENDA VITANI PAMOJA NA ASKARI WAKE.

“Hata ikawa, mwanzo wa mwaka mpya, wakati watokapo wafalme kwenda vitani, Daudi akampeleka Yoabu, na watumishi wake pamoja naye, na Israeli wote, wakaangamiza wana wa Amoni, wakakuhusuru Raba. LAKINI DAUDI MWENYEWE AKAKAA YERUSALEMU”. (2 Samweli 11:1)

          Kama kiongozi wao, Daudi alitakiwa kuongozana na watu wake vitani, lakini yeye aliamua kubaki Yerusalemu asiende vitani, na akamtuma mtu mwingine amwakilishe. Na jambo hili lilimpa nafasi nzuri sana ibilisi ya kumpa Daudi kazi nyingine ya kufanya. Ni kazi gani hiyo?

“Ikawa wakati wa jioni, Daudi akaondoka kitandani, AKATEMBEA JUU YA DARI ya jumba la mfalme; na alipokuwa juu ya dari aliona mwanamke ANAOGA; naye huyo mwanamke alikuwa MZURI SANA WA KUPENDEZA MACHO”. (2 Samweli 11:2)

Ni kitu gani kilimfanya Mfalme Daudi aamue kutembea juu ya dari ya jumba lake badala ya kwenda vitani pamoja na watu wake? Na alipomwaona Bathsbeba, mkewe Uria akioga alishindwa kujizuia, mwisho wake ni kuzini naye na huyo mama kupata mimba!

Wakristo wengi wamejikuta wameingia katika mtego wa zinaa kwa sababu ya kutokwenda ‘Vitani’ wakati wanapotakiwa kufanya hivyo. Vita tunavyovisema, si vita vya kimwili.

“Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili, maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome; tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikra ipate kumtii Kristo”. (2 Wakorintho 10:3,4)

Na pia imeandikwa; “ Kwa maana kushindani kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili juu ya majeshi ya pepo wabaya, katika ulimwengu wa roho”. (Waefeso 6:11)

Ndiyo maana Yesu Kristo alisema; “ Kesheni mwombe msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.” (Mathayo 26:41)

Usipovipiga vita katika maombi, inakuwa ni rahisi sana kuangushwa na majaribu unapokutana nayo. Wakristo wakipoa katika maombi inakuwa rahisi kuanguka katika dhambi, si katika zinaa peke yake, bali katika mtego wowote ambao shetani anauweka mbele yao!
Kutokuwa mwombaji, ni sawa na kutokwenda vitani na wenzako, kama vile Mfalme Daudi alivyofanya.

Kwa hiyo unaona ya kuwa ingawa Mfalme Daudi alikuwa mtu wa Mungu, mtumishi wake, na mpakwa mafuta wake, alianguka katika zinaa. Na hata hivi leo kuna wakristo, tena wameokoka, na kupakwa mafuta kwa Roho Mtakatifu, wanaonguka katika dhambi ya zinaa. Kwa nini? Kwa kuwa hawavipigi vita vya kiroho na wenzao, na wamepoa katika kumtumikia Bwana.

Je! Lutu aliangukaje?

Hili ni swali ambalo Roho Mtakatifu aliniuliza baada ya kunieleza habari za Mfalme Daudi. Ingawa Lutu alikuwa mtu wa Mungu, na licha ya kuwa alikuwa anabebwa kwa maombi ya Ndugu yake Ibrahimu, bado alianguka katika zinaa.

Roho Mtakatifu alikuwa anaendelea kunijibu swali nililokuwa najiuliza ya kuwa, watu waliookoka wanaangukaje katika zinaa?

Habari za kuanguka kwa Lutu zimeandikwa katika kitabu cha Mwanzo 19:30-38.

Lutu alizini na watoto wake wawili wa kike baada ya kuleweshwa mvinyo.
Na ukiisoma habari hii inasikitisha sana. Shetani alipata nafasi ya kumwangusha Lutu si kwa sababu ya binti zake kumlewesha mvinyo, bali kwa kuwa MKE WAKE HAKUWA PAMOJA NAYE. Unadhani mke wake angekuwapo hawa watoto wangepata nafasi ya kumlaghai baba yao? Hapana! Kwa nini?
Kwa maana “ Bwana ameumba jambo jipya duniani, mwanamke atamlinda mwanaume.” (Yeremia 31:22)

Unaweza kujiuliza ni kwa njia gani mke atalimnda mume wake. Kumbuka imeandikwa mke mwenye busara, mtu hupewa na Bwana. Kazi moja ya busara iliyo ndani ya mke ni kumlinda mume kutokana na mashambulizi ya Malaya! Soma Mithali 2:11-22.

Hata hivi leo ndoa ambazo mume na mke hawakai vizuri, huwa ni rahisi kwa wao kuanguka katika dhambi ya zinaa hata kama wameokoka. Na huu siyo ushuhuda mzuri.
Tunamshukuru Mungu kwa wale ambao wamesimama katika ushuhuda ingawa ndoa zao zina matatizo.

Jambo la kujifunza zaidi

Roho Mtakatifu alipokuwa anaendelea kunifundisha akasema ndani ya moyo wangu hivi; “Watu wengi wanadhani zinaa ni tendo la kimwili tu linalofanywa kati ya mwanaume na mwanamke nje ya ndoa, lakini kuna namna zaidi ya moja unayoweza kuanguka katika zinaa.”

Niliposikia hivyo moyoni mwangu, niliichukua Biblia na nikaanza kuisoma upya juu ya zinaa na nikaona kuna namna nne ambazo zinaa inatajwa:-

1.     KATIKA MWILI:
“….Lakini mwili si kwa zinaa, bali ni kwa Bwana, naye Bwana ni kwa mwili. Je! Hamjui ya kuwa miili yenu ni viungo vya Kristo? Basi nivitwae viungo vya Kristo na kuvifanya viungo vya Kahaba? Hasha! Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? …. Ikimbieni zinaa, kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe. Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu.” (1 Wakorintho 6:13-20)

2.     KUTAMANI KWA MACHO. Yesu Kristo alisema;
“Mmesikia kwamba imenenwa Usizini; lakini mimi nawaambia, kila mtu AMTAZAMAYE MWANAMKE KWA KUMTAMANI, amekwisha KUZINI NAYE MOYONI MWAKE.” (Mathayo 5:27,28)

3.     KUACHA MKE NA KUOA MWINGINE
Yesu Kristo alisema;
“Kila amwachaye mkewe na kuoa mke mwingine azini ……” (Luka 16:18)

4.     KUOA ALIYEACHWA. Yesu Kristo alisema;
“Kila amwachaye mkewe na kumwoa mke mwingine azini; NAYE AMWOAYE YEYE ALIYEACHWA NA MUMEWE AZINI.” (Luka 16:18)

          Kila mtu na ajipime katika hayo; ikiwa umefanya mambo kama hayo niliyoyataja, biblia inasema UMEZINI! Je       Hakuna waliokoka wanaofanya mambo ya jinsi hii? Wanaowaacha wake zao halali? – Wanaooa walioachwa? – na wanaozini katika mwili?